Harambee ya Waziri Mkuu yakusanya shilingi 138.2m

screen-shot-2016-12-31-at-7-35-29-pm

Jumla ya shilingi milioni 138.26 zimechangwa katika harambee ya papo kwa papo iliyoendeshwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari wilayani Ruangwa.

Hatua hiyo inafuatia wingi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza Januari 2017 lakini hawakufanikiwa kupata nafasi katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa Vyumba vya madarasa pamoja na ukosefu wa makazi ya walimu.

Katika Harambee hiyo iliyofanyika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ruangwa Waziri Mkuu amefanikisha kupatikana kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 120.65, mifuko 550 ya saruji na mabati 360 vyenye thamani ya shilingi milioni 17.61 ambavyo vitatumika kujenga madarasa manne ya kidato cha kwanza yanayotakiwa kuwa yamekamilika ifikapo Januari 15, 2017.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue, jumla ya watoto 319 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikosa nafasi sababu ya ukosefu wa madarasa na kutakiwa kusubiri chaguo la pili ambalo kwa kawaida hufanyika Februari, kila mwaka

Katika Hatua nyingine Waziri Mkuu alizindua Jengo la CCM wilaya ya Ruangwa baada ya kukarabatiwa ambalo litakuwa na ukumbi utakaotumika pia kibiashara

Facebook Comments