Polepole asema CCM Inahitaji viongozi waliojikita katika imani ya chama

screen-shot-2016-12-31-at-7-34-24-pm

Chama cha Mapinduzi CCM kimesema kinatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ili kuwapata viongozi waliojikita katika imani ya Chama hicho hususan ya kupiga vita rushwa na Ufisadi ili kukirejesha chama hicho kwa wananchi kutoka ngazi ya chini ikiwa ndiyo msingi na lengo la kuanzishwa chama hicho.

Katibu Itikadi na Uenezi Taifa wa Chama cha Mapinduzi Humprey Polepole, akizungumza na jumuiya ya vijana kutoka vyuo vya elimu ya juu jijini dar es salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amesema Misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho iliachwa na baadhi ya viongozi na hivyo kusababisha wananchi kugawanyika.

Aidha amesema CCM mpya ambayo iko mbioni kusukwa haitokuwa na muhali kwa mwanachama atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika kuwania nafasi yeyote.

Aidha Bwana Polepole amesema CCM itaendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake katika kutetea haki za wananchi wanyonge lakini pia CCM itaendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wake Rais Dk. John Pombe Magufuli na serikali yake katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na Ufisadi na katika kuwatetea wananchi wanyonge.

Facebook Comments