Rais Dkt. Magufuli aagiza wizara ya fedha kutoa Bilioni 40.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kumalizia madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki baada ya Serikali kununua korosho za wakulima katika msimu wa mwaka 2018/19.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho, katika kikao kilichohudhuriwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Pamoja na kuagiza Wizara ya Fedha na Mipango itoe fedha hizo kesho Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wakulima na sio vinginevyo, lakini pia kuhakikisha wanalipwa wakulima wanaostahili kupata malipo hayo.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao kumetokea wizi mkubwa wa fedha za wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) hali iliyosababisha wakulima wengi kuishi maisha duni.

Mhe. Rais Magufuli amesema amesikitishwa kuona viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia wakulima mpaka alipoamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jenerali John Mbungo ambaye kwa muda mfupi amebaini kuwepo wizi wa shilingi Bilioni 1.23 na tayari amefanikisha kurejeshwa kwa shilingi Milioni 375 katika Mkoa wa Lindi pekee.

Amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa ipasavyo kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.

Kuhusu minada ya korosho, Mhe. Rais Magufuli ametaka utaratibu uliowekwa wa kufungua mnada kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 Jioni na kisha kufungua masanduku yenye zabuni kwa uwazi mara baada ya saa 10 jioni uheshimiwe, ili kuepusha njama za upangaji wa bei.

Viongozi wa Mikoa na Wilaya wamemuahidi Mhe. Rais Magufuli kuwa wanakwenda kusimamia maelekezo yake na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa.

Comments

comments

clement

Read Previous

Mkutano wa AfDB umekubali na kuridhia ongezeko la mtaji.

Read Next

Saluni Dar es Salaam zajihusisha na Biashara ya Vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!