Mkutano wa Mawaziri sekta ya Afya na Ukimwi nchi za SADC.

Tanzania ni miongoni mwa nchi saba duniani zilizofikia malengo ya mkakati wa kutokomeza kifua kikuu (TB) ifikapo mwaka 2020, ambapo katika mwaka 2018, maambukizi mapya ya kifua kikuu yalipungua kwa asilimia 4.6 huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikipungua kutoka vifo 55,000 mwaka 2015 hadi vifo 39,000 2018 ambayo ni sawa na asilimia 27.

Hayo yamebainishwa na makamu wa Rais wa Jmuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua mkutano wa pamoja wa mawaziri wanaosimamia sekta ya afya na ukimwi wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC, ambapo amesema utoaji wa taarifa za wenye TB pia umeongezeka kwa asilimia 20.6 kutoka mwaka 2015 hadi 2018, hii ikitokana na kuongezeka kwa kiwango cha utambuzi wa ugonjwa huo kutoka asilimia 37 mwaka 2015 na kufikia asilimia 53 mwaka 2018.

Kwa upande wa ugonjwa wa UKIMWI mama Samia amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya kwa kiwango cha asilimia 20.6 kutoka mwaka 2015 hadi 2018 kwa walio na umri zaidi ya miaka 15 na asilimia 31.3 kwa walio chini ya umri huo.

Awali akimkaribisha makamu wa rais, waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu, ameelezea jitihada zinazofanywa na nchi wanachama wa SADC katika kutekeleza maazimio ya SADC ya afya na ukimwi yanayolenga kukinga, kupunguza na kutokomeza magonjwa katika ukanda wa SADC kwa kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma bora za afya.

Mkutano wa mawaziri wa afya na ukimwi wa SADC uliobeba kauli mbiu isemayo “ushirikiano wa nchi za SADC ni nguzo kuu kufikia maendeleo endelevu ya sekta ya Afya na mapambano dhidi ya UKIMWI” ulitanguliwa na mkutano wa wataalamu wa kisekta ambao walikutana kwa siku tatu kwa ajili ya kujadili na kutoa mapendekezo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya na UKIMWI, mapendekezo ambayo yapo mikononi mwa mawaziri wenye dhamana kwa ajili ya kuyatolea maamuzi na utekelezaji.

Comments

comments

Anthony Shija

Read Previous

Uchunguzi dhidi ya Rais Trump kuanza Novemba 13.

Read Next

Rais Dkt. Magufuli amesisitiza ushirikiano Kiuchumi nchi za Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!