Dkt. Shein azindua daraja la Kibonde Mzungu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ujenzi wa barabara na daraja la Kibonde Mzungu ni uthibitisho wa Mapinduzi kwani kabla ya Mapinduzi hapakuwepo madaraja na barabara nzuri kama zinazojengwa hivi sasa Zanzibar.

Rais Dkt. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya ufunguzi wa Daraja la Kibonde Mzungu, lililopewa jina “Daraja la Dkt. Shein”, lililopo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyofanyika eneo hilo la Kibonde Mzungu ikiwa ni shamrashamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Shein alieleza kwa ufupi historia ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kueleza juhudi zilizochukuliwa katika kuhakikisha wanyonge wa Zanzibar wanakuwa huru sambamba na kuimarika kwa sekta za maendeleo zikiwemo barabara.

Rais Dkt. Shein alisema kuwa Mapinduzi yataendelea kusemwa kila siku kwani ni jambo ambalo lina maslahi ya wananchi wote licha ya kuwepo baadhi ya watu ambao hawapendi kuyataja, kuyazungumza wala kuyasikia.

Alisema kuwa ndani ya miaka 56, kumefanywa mambo mengi na Zanzibar sivyo ilivyo leo huku akisisitiza kuwa kila fedha zitakaporuhusu, zitajengwa barabara hata barabara za juu (Fly-over).

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Shein alikubali Daraja hilo kuitwa jina lake na kupokea heshima hiyo na kumpongeza Waziri, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo kwa kushirikiana na mkandarasi wa ujenzi huo.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dkt. Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa ilikuwa ni changamoto kubwa sana hasa wakati wa mvua na maji yalikuwa yanajaa katika eneo hilo na kusababisha madhara ambapo kwa sasa tatizo hilo limeondoka na litakuwa ni historia na wananchi hivi sasa wanapita usiku na mchana.

Comments

comments

Anthony Shija

Read Previous

Marekani yaelezea utayari kufanya mazungumzo na Iran.

Read Next

Ukraine yaamini ndege ilitunguliwa na kombora la Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!