Iran yaikaribisha kampuni ya Boeing kushiriki uchunguzi.

Iran imeikaribisha kampuni ya Boeing ya Marekani, kushiriki katika uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali ya ndege ya Ukraine iliyoanguka karibu na uwanja wa ndege wa Tehran mwanzoni mwa wiki hii na kuua watu wote 176 waliokuwemo.

Hatua hiyo inakuja wakati viongozi wa nchi za magharibi wakidai kuwa ndege hiyo iliangushwa na kombora lililofyatuliwa kimakosa na Iran saa chache baada ya nchi hiyo kuzishambulia kambi za jeshi la Marekani nchini Iraq, kulipiza kisasi mauaji ya jenerali wake, Qasem Soleimani.

Shirika la habari la Iran, IRNA, limemnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje Abbas Mousavi, akisema Iran imeialika pia Ukraine na nchi nyingine ambazo raia wao wengi walipoteza maisha katika ajali hiyo kwenda Iran kushiriki katika uchunguzi.

Iran inasisitiza ndege hiyo ilianguka kutokana na hitilafu za kiufundi. Awali Iran ilikataa kuiruhusu kampuni ya Boeing kushiriki katika uchunguzi wa ajali hiyo.

Wakati huo huo Baraza la Wawakilishi la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Democratic limepitisha azimio lisilo na nguvu kisheria la kuweka ukomo katika uwezo wa rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran.

Azimio hilo linamtaka Rais Trump kusitisha mipango yote ya kijeshi dhidi ya Iran hadi pale bunge litakapoidhinisha kuingia vitani na nchi hiyo au kuruhusu matumizi ya nguvu za kijeshi kuzuia mashambulizi dhidi ya Marekani.

Comments

comments

Anthony Shija

Read Previous

Dampo la Stesheni lafungwa rasmi.

Read Next

Wahofia usalama wa afya kutokana na kutiririka majitaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!