China yaitaka Marekani iheshimu juhudi za China za kupambana na virusi vya korona na kutarajia kuona msaada kufika mapema.

China imeitaka Marekani isichukue hatua kupita kiasi kufuatia maambukizi ya virusi vipya vya korona, na badala yake kuyaangalia kwa usahihi na utulivu, kuheshimu na kuratibu juhudi za China katika kukinga na kudhibiti virusi hivyo, na kushirikiana na China na jamii ya kimataifa kupambana na maambukizi hayo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bibi Hua Chunying ameyasema hayo leo hapa Beijing akizungumzia kauli aliyotoa rais Donald Trump wa Marekani jana, kuwa kimsingi Marekani imefunga mlango kwa watu kutoka China na haitawaruhusu maelfu ya watu walioambukizwa virusi kuingia nchini humo. Rais Trump pia alisema uhusiano kati ya Marekani na China ni mzuri, na Marekani inatoa msaada mkubwa kwa China.

Bibi Hua amesema hivi sasa serikali ya China na watu wake wanafanya kila wawezalo kupambana na maambukizi ya virusi vya korona, na juhudi hizo zimeanza kuonesha ufanisi wake. Amekiri kuwa watu walioambukizwa virusi vya korona ni wengi, lakini kiwango cha vifo ni asilimia 2.1 tu, ambacho ni chini sana kuliko magonjwa ya kuambukizwa kama Ebola, SARS na MERS, na kwamba hivi sasa kiwango cha kupona kinaendelea kuongeza. Amesema China ina imani na uwezo wa kushinda vita hivyo.

Bibi Hua ameongeza kuwa Marekani imeeleza mara nyingi kuwa itatoa misaada kwa China, na China inatarajia kupokea misaada hiyo mapema iwezekanavyo.

Wakati huohuo, kauli zilizotolewa hivi karibuni na waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross kuwa mlipuko wa virusi vya korona unaweza kurudisha nafasi za ajira Marekani zimekosolewa na wengi, wakimsema kuwa kiongozi huyo “anakosa ubinadamu” na hafahamu mambo ya uchumi.

Mhariri wa shirika la habari la Bloomberg Noah Smith amesema, sio ubinadamu kusema hivyo wakati maelfu ya watu wanaambukizwa virusi huku mamilioni ya watu wakijifunga nyumbani kuepuka maambukizi hayo. Amesema maambukizi yanaweza kufanya makampuni ya kimataifa kufikiria tena mkakati wao nchini China, lakini hayatafanya nafasi za ajira zirudi Marekani.

Naye mshindi wa tuzo ya Nobel na mhariri wa gazeti la New York Times Paul Krugman pia amekosoa kauli ya waziri huyo wa biashara akisema, ni wazi kuwa Ross na wafanyakazi wenzake hawafahamu mambo ya uchumi. Amesema uzalishaji wa kisasa sio kama uzalishaji wa vizazi kadhaa vilivyopita, ambapo sekta za viwanda za nchi tofauti zilikuwa zikishindana moja kwa moja.

Nalo Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG limetoa tahariri likisema kauli ya waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross iliyotaka kuinufaisha Marekani kutokana na maambukizi hayo nchini China imeonesha ubinafsi mkubwa wa wanasiasa wa Marekani, ambao wanaona kuwa chochote kinachoumiza China kinanufaisha Marekani. Vilevile tahariri hiyo imesema, waziri Ross hana ujuzi wa kimsingi wa uchumi, wala hatambui mlolongo wa uzalishaji bidhaa duniani ambapo nchi tofauti zina nguvu bora tofauti na zinapaswa kushirikiana kwa kusaidiana na kunufaishana ili kuendeleza biashara ya dunia. Tahariri hiyo inasema maambukizi hayo yataathiri uchumi wa China, lakini ni kwa muda mfupi, na uchangamfu na uhai wa kipekee katika soko la China utakuwa wa muda mrefu, na msingi wa ukuaji wa uchumi wa China hautabadilika.

Comments

comments

Anthony Shija

Read Previous

Mahakama nchini Afrika Kusini yatoa hati kukamatwa kwa Zuma.

Read Next

Mvua zakatisha masomo ya wanafunzi 350 Handeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!