Aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura amesomewa mashitaka 17 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini DSM ikiwemo utakatishaji fedha wa Mil.75.

Katika kesi hiyo Wambura anakabiliwa na shtaka moja la kughushi, Shtaka moja la kutoa nyaraka za uongo, mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali George Barasa akisaidiana na Moza Kasubi pamoja na Imani Mitumezizi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, inadaiwa mshtakiwa alitenda kosa la kughushi Julai 6,2004 mahali pasipo julikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Katika shtaka la kutoa Nyaraka ya uongo inadaiwa, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba ya tarehe 6/7/2004 akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck system Ltd akidai kuwa anadai mkopo wa dola za kimarekani elfu 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Aidha katika shtaka la 3 hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia jumla ya zaidi ya Sh.Milioni 95 kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbalimbali na riba kutoka kwa Jek huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi ambapo mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza.

Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kumsomea Wambura mashtaka yake, wakili wa utetezi Majura Magafu aliiomba mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo kwa sababu mashtaka yote 17 hakuna shtaka hata moja lilolofunguliwa chini umya sheria ya uhujumi uchumi hivyo yalitakiwa yafunguliwe kama mashtaka ya kesi ya kawaida ya jinai ambayo yanamruhusu mshtakiwa kujibu.

Kufuatia hoja hiyo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 14 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi.


Comments

comments