Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyotembelea eneo la mradi wa kuzalisha umeme wa Stigler’s Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani imeelezea kuridhishwa na hatua za awali za utekelezaji mradi huo.

Katika eneo hilo kamati hiyo imejionea kazi za miundombinu-wezeshi ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na nguzo za umeme kwenye mradi huo ambao unaratajiwa kutumia zaidi ya shilingi trilioni 6.5 na kuzalisha umeme megawati 2,115 utakapokamilika.

Akiongea mara baada ya kamati ya kudumu ya bunge ya madini na nishati kutembelea eneo la mradi wa kuzalisha umeme Wilayani Rufiji mkoani Pwani, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya nishati na madini Dunstan Kitandula amesema mradi huo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi na wameridhika na hatua iliyofikiwa huku waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akisema kazi za ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi zimekamilika ambapo kwa sasa makandarasi wanaendelea na ujenzi wa eneo ambalo litatumika kwa ajili ya makazi ya wahandisi na eneo la kuhifadhia vifaa vitakavyotumiwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Wabunge wa kamati ya kudumu ya nishati na madini wamekagua ujenzi wa reli ya tatu katika kituo kidogo cha treni cha Fuga ambayo itatumika kupokea mizigo ya vifaa vya ujenzi wa miradi huo na kuridhishwa na shirika la umeme kwa kufikisha umeme kwa asilimia 100 katika eneo la mradi.

Comments

comments