Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mazungumzo ‘ya kina’ na Rais wa Urusi Vladimir Putin pembezoni mwa mkutano wa kilele wa nchi zinazounda kundi la mataifa yanayoongoza kiuchumi duniani, G20 nchini Argentina.

Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert amesema mada kuu ilikuwa mzozo unaozidi kupanuka kati ya Urusi na Ukraine.

Kansela Merkel ameitaka Urusi kuwaachia mabaharia wa Ukrane waliokamatwa na wanajeshi wa majini wa Urusi tangu Jumapili iliyopita.

Urusi pia ilikuwa imetakiwa kufanya hivyo na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye aliketi pamoja na Rais Putin kabla ya Bi Merkel.

Hata hivyo Rais Putin amewaambia viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa, kwamba suala la mabaharia hao wa Ukraine linashughulikiwa na mahakama.

Katika mkutano na waandishi wa habari baadaye, Rais Putin alinukuliwa akisema rais wa Ukraine Petro Poroshenko hana utashi wa kupata suluhisho la amani, na kuonya kuwa vita hivyo vitaendelea kuwepo muda wote kama chama alichokiita cha kivita kitakapoendelea kuwepo madarakani nchini Ukraine.

Comments

comments