Korea Kaskazini yadai Marekani inachochea Mvutano wa Kijeshi.

Korea Kaskazini imeinyooshea kidole Marekani kwa madai ya kuchochea mvutano wa kijeshi kutokana na mazoezi ya kijeshi inayofanya ikishirikiana na Korea Kusini ambapo imetahadharisha kuwa italazimika kuchukua hatua za kujihami.

Balozi wa Korea Kaskazini mjini Geneva amewaambia wajumbe wanaoshiriki mkutano wa kupunguza silaha unaodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kwamba Korea Kaskazini itafikiria upya hatua ilizochukua hadi sasa katika kujiimarisha zaidi.

Hata hivyo, mjumbe wa Marekani kwenye mkutano huo, Robert Wood, amekanusha madai hayo ambapo amesema Marekani haichochei mivutano yeyote ambayo ni hatarishi kwa usalama.

Bwana Wood amesema kuwa Marekani imedhamiria kutekeleza lengo la kuondolewa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini kama jinsi kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, alivyokubaliana na Rais Donald Trump kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika Singapore mwaka uliopita.

Mjumbe huyo wa Marekani amesema nchi yake inasubiri kwa hamu kubwa kurejea kwenye mazungumzo na Korea Kaskazini ili kutekeleza lengo lililowekwa kwenye mkutano huo.

Comments

comments