Kufuatia malalamiko ya abiria wanaotumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam kuhusu ugumu wa usafiri huo, serikali imeingilia kati ili kupata ufumbuzi wa haraka wa kukabiliana na hali hiyo huku ikisema imeunda timu maalumu inayofanya mapitio ya namna bora ya kuboresha mradi huo.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa – TAMISEMI Seleman Jaffo amemwagiza mtendaji mkuu wa wakala wa mabasi yaendayo haraka – DART Mhandisi Leornard Lwakatare ahakikishe kwamba mabasi 10 yanayofanya safari za kimara – Mbezi kuyahamishia Kimara – Kivukoni na Gerezani ili kuwapunguzia abiria adha inayowakabili.

Katika kukabiliana na upungufu utakaojitokeza kwa abiria wa Mbezi – Kimara amemwelekeza Mhandisi Lwakatare kushirikiana na mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini – Sumatra kuongeza mabasi ya kawaida yatakayotoka Kimara kwenda Mbezi.

Aidha ameitaka DART kuhakikisha kwamba UDART ambao ndio waendeshaji wa mradi huo kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya mabasi yake ili kuondoa usumbufu unaojitokeza wa upungufu wa mabasi pamoja na kumtaka mtendaji mkuu DART kuwasilisha majina ya watendaji wake kwa katibu mkuu TAMISEMI ambao anahisi ni kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya siku saba ili wafanyie marekebisho kwa maslahi mapana ya Taifa.

Waziri Jaffo amekiagiza kitengo cha TEHAMA kutafuta namna ya kutumia kadi badala ya tiketi za karatasi jambo ambalo linapoteza mapato.


Comments

comments