Mamlaka ya kuratibu safari za anga za Marekani, FAA, imesema haitasimamisha safari za Ndege aina ya Boeing 737 Max, kufuatia ajali ya Ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia iliyosababisha vifo vya watu 157.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kaimu afisa mkuu wa mamlaka hiyo, Dan Elwell, alisema Jumanne kwamba uchunguzi uliofanywa kufikia sasa, haujabaini hitilafu yeyote katika mfumo wa Ndege hizo na kwa hivyo haoni haja ya kusitisha safari zake.

Ajali hiyo imesababisha baadhi ya mashirika ya ndege ya nchi kadhaa kusitisha safari za ndege hizo za Boeing 737 MAX zikiwemo China, Uingereza na Ethiopia.

Mashirika matatu ya Ndege nchini Marekani, Southwest Airlines, American Airlines na United Airlines yamesema Ndege hizo za 737 Max zitaendelea na safari licha ya baadhi ya abiria kuandika ujumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, wakilelezea hofu yao. Hayo yamejiri katika siku ambayo mamlaka ya usafiri wa anga ya Umoja wa ulaya ilipotangaza marufuku ya ndege hizo katika anga za nchi wanachama wake.

Jumanne wiki hii maombolezi yameendelea huku salamu za rambirambi zikiendelea kutolewa kwa jamaa za watu 157 waliopoteza maisha yao ndege hiyo ya shirika la ndege la Ethiopia ilipoanguka karibu na Addis Ababa siku ya Jumapili.

Comments

comments