Burundi imetoa waranti ya kimataifa wa kumkamata rais wake wa zamani Pierre Buyoya na maafisa wengine 16, kuhusiana na mauaji ya Melchior Ndadaye, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Burundi Sylvestre Nyandwi amesema uchunguzi umebainisha kuwa watu hao walihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya Ndadaye, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, wa kwanza pia kutoka jamii ya Wahutu.

Mauaji hayo yalifuatiwa na machafuko makubwa ya kikabila, ambamo watu zaidi ya 300,000 waliuawa. Buyoya kwa wakati huu ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali, na ni mtu anayeheshimiwa barani Afrika na katika jumuiya ya kimataifa .

Buyoya, Mtutsi aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987 alikubali kushindwa na Ndadaye katika uchaguzi wa mwaka 1993.

Lakini Ndadaye alihudumu madarakani kwa miezi minne tu, akauawa na kundi la wanajeshi Watutsi wenye misimamo mikali, katika jaribio la mapinduzi lililoitumbukiza Burundi katika mzozo ambao athari zake zinaendelea hadi leo.

Comments

comments