Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope, amesomewa mashtaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuachiwa kwa dhamana.

Hanspope ameunganishwa katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu”.

Baada ya kuunganishwa katika kesi hiyo yeye na wenzake walisomewa mashtaka 10 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro.

Katika mashitaka hayo 10, Hanspope anakabiliwa na mashtaka 2, ikiwemo kuwasilisha nyaraka za uongo ambapo pia anakabiliwa na makosa ya kughushi.

Katika mashtaka hayo 10, yamo ya kula njama, kutoa nyaraka za uongo, matumizi mabaya ya madaraka, kughushi, utakatishaji, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kuendesha biashara bila kufuata sheria.

Katika shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, anadaiwa March 15, mwaka 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. Milioni 400 wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shitaka la kughushi linalowakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28 mwaka 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya dola 40,577, zaidi ya Sh. Milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shitaka jingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30 mwaka 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Hata hivyo, shitaka la mwisho halikusomwa kwa sababu linamuhusu mshtakiwa wa 4 ambaye bado hajafikishwa mahakamani.

Baada ya kueleza hayo, Mahakama ilitoa masharti ya dhamana kwa Hanspope ya kuwa na wadhamini 2, watakaosaini Bondi ya Sh.MIL 15 kila mmoja, ambapo walitimiza masharti hayo na kesi imeahirishwa hadi October 19 mwaka 2018.

Tazama Video hapa Chini;

Comments

comments