Naibu Waziri ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kumsimamisha kazi mara moja mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, Daniel Kingu, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kumsimamisha kazi mara moja mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, Daniel Kingu, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja jijini humo.

Dkt. Kijaji ametoa maagizo hayo kufuatia ziara ya kushitukiza aliyoifanya kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine na kumtaka ampelekee shilingi laki 7 za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki (EFD Machine) la sivyo angefungiwa biashara yake.

Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amewataka watendaji wa TRA kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao, kukadiria kodi kwa haki, watumie lugha nzuri kwa wateja na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa isiyolipika.

Comments

comments