Mafua ya ndege hayajaingia nchini Serikali yataka wananchi kuchukua tahadhari

1040806_tcm9-284943

Serikali imesema ugonjwa wa Mafua ya Ndege ambao umeingia nchini Uganda, bado haujaingia hapa nchini, na kuwataka wananchi kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mara moja waonapo vifo vya ndege au kuku.

Ugonjwa wa mafua ya Ndege umegundulika baada ya kuwepo kwa vifo vingi vya ndege pori katika maeneo ya nchini Uganda. Vilevile, vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalim katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo amesema kuwa Wizara inaandaa Timu kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo ili timu hiyo iweze kwenda kujenga uwezo wa kamati za kudhibiti milipuko ya mgonjwa na majanga hususani kwenye mkoa wa Kagera na mkoa wa Mwanza.

taarifa hiyo imeeleza kuwa Timu hiyo pia itashirikiana na Timu za Mikoa kuandaa Mpango Mkakati wa Kudhibiti Ugonjwa huu usiingie ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo ya kuboresha ikiwemo upatikanaji wa vifaa kinga.

Ugonjwa wa Mafua ya Ndege unasababishwa na virusi vya aina ya Influenza na huenezwa na ndege pori wanaohama hama.

Binadamu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu. Hivyo serikali inashauri wananchi kutokugusa mizoga ya ndege pori au kinyesi chake. Maambukizi ya ugonjwa huu yanaweza pia kutoka kwa ndege pori na kuathiri jamii ya kuku na bata na ndege ambao wanafugwa nyumbani.

Dalili za ugonjwa wa mafua ya ndege ni pamoja na homa kali, kutokwa na makamasi mepesi pamoja na mafua, kuumwa na kichwa, kukohoa, vidonda kooni, kupumua kwa shida na vichomi. Vilevile baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na dalili kama kuharisha, kutapika, kuumwa na tumbo na kutokwa na damu puani na kwenye ufizi.

Comments

comments