Rais wa Marekani Donald Trump amefuta mkutano wa mazungumzo kati yake na Rais wa Urusi Vladmir Putin aliopanga kuufanya kando na mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri zaidi duniani G20.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema sababu ya kufuta mkutano huo ni hatua ya Urusi kuendelea kuzishikilia meli za kivita za Ukraine zilizokuwa zikifanya doria kwenye eneo la Crimea hatua inayoongeza mvutano wa kiusalama baina ya mataifa hayo.

Aidha Viongozi wa mataifa 20 tajiri zaidi duniani wameendelea kuwasili jijini Buenos Aires nchini Argentina, ikiwa ni mkutano wa kwanza wa aina hiyo kufanyika katika bara la Amerika ya Kusini.

Viongozi hao wanatarajiwa kuangazia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa hali ya uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabia nchi na usalama. Hata hivyo mambo kadhaa yanatarajiwa kujitokeza ikiwa ni pamoja na mvutano wa kibiashara baina ya China na Marekani, shinikizo kwa kiongozi wa Saudi Arabia Mwanamfalme Mohammed Bin Salman kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Comments

comments