Rais Dkt. Magufuli amewataka wachezaji wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kuongeza juhudi za kupata ushindi katika michuano mbalimbali inayoshiriki

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wachezaji wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kuongeza juhudi za kupata ushindi katika michuano mbalimbali inayoshiriki ikiwemo ya kufuzu fainali za michuano ya Afrika (AFCON) itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo alipokutana na kuzungumza na wachezaji wa Taifa Stars na viongozi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Ikulu Jijini Dar es Salaam, na kuwataka wachezaji kujenga umoja na kutanguliza maslahi ya Taifa wanapochezea timu hiyo badala ya maslahi ya timu zao.

Rais Magufuli ambaye ameichangia Taifa Stars shilingi Milioni 50 na baadaye kula chakula cha mchana na wachezaji hao, amesema kiu yake na kiu ya Watanzania ni kuona timu yao inapata ushindi na kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kwamba matokeo mabaya ya timu hiyo hukatisha tamaa.

Aidha, Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya matumizi mabaya ya fedha, rushwa na uongozi mbaya katika vyama vya michezo hali iliyosababisha TFF kunyimwa fedha za ruzuku kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ambapo amewataka viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, TFF na BMT kushugulikia dosari hizo ili Tanzania iendelee kupata ruzuku hiyo.

Katika shukrani zao Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Ledegra Tenga na Rais wa TFF Wallace Karia wamemueleza Rais Magufuli namna walivyojipanga kushirikiana na wadau kuhakikisha timu hiyo inafuzu kucheza AFCON pamoja na timu nyingine za Taifa zinazojiandaa kwa michuano ya kimataifa ambazo ni Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes, Kilimanjaro Heroes na Twiga Stars.

Aidha Kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike na Kipa namba moja wa timu hiyo Aishi Manula nao wamemuahidi Rais Magufuli kuwa watapambana kuhakikisha wanafuzu kucheza AFCON mwakani, ikiwa ni miaka 38 tangu Tanzania ilipofuzu kucheza michuano hiyo mwaka 1980.

Comments

comments