Rais Dkt. John Pombe Magufuli, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Urusi ulioongozwa na Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mikhail Bogdanov, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi hiyo na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza inatambua umuhimu wa uhusiano huo na kwamba itauendeleza na kuukuza zaidi hususani katika masuala ya biashara, uwekezaji, utalii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na miundombinu.

Kwa upande wake Bwana Bogdanov ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kasi nzuri ya maendeleo katika kipindi kifupi na amebainisha kuwa Urusi imedhamiria kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Amesema hivi karibuni Tanzania na Urusi zitatiliana saini makubaliano ya kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission ) katika biashara, uwekezaji na uchumi ili rasilimali na fursa zilizopo katika pande zote zitumike kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi amesema kwamba Tanzania inatarajia tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Urusi itasaidia kukuza uchumi.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Tanzania na Misri wanaoshughulikia ujenzi wa uwanja wa michezo unaotarajiwa kujengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morocco jijini Dodoma.

Balozi wa Morocco hapa nchini aliyeongoza ujumbe wa wataalamu kutoka Morocco Abdelilah Benryane amesema pamoja na kuzungumzia uhusiano mzuri wa Tanzania na Morocoo wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco hapa nchini mwaka 2016 ikiwemo ujenzi wa Msikiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Jijini Dar es Salaam na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema uwanja huo utajengwa eneo la Nanenane kando ya barabara ya Dodoma – Morogoro, utajengwa kwa mfano wa mlima Kilimanjaro na utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya 85,000 na 100,005.

Comments

comments