Serikali kupitia Wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, inatarajia kutatua mgogoro wa wananchi wanaodaiwa kuvamia maeneo ya uwanja wa ndege wa Mwanza kwa kuwalipa fidia, ili kupisha upanuzi wa uwanja huo, unaotarajiwa kujengwa kwa hadhi ya kimataifa.

Uamuzi wa Serikali wa kutaka kuwalipa fidia wananchi hao, vilevile utasaidia kutatua kilio kuhusu hatma ya wananchi wa maeneo hayo, baada ya kudaiwa kuwa maeneo wanayoishi waliyavamia kinyume cha sheria.

Akiwa katika ziara ya ukaguzi wa maeneo yanayozunguka uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano mhandisi Isack Kamwelwe, amesema ziara yake inalenga kujiridhisha kuhusu mgogoro wa uvamizi huo, uliodumu takribani miaka 40 iliyopita.

Katika ziara yake pia akazungumzia suala la Taifa kunufaika kiuchumi, baada ya ndege za Shirika la ndege Tanzania (ATC), kuanza kusafirisha minofu ya samaki kutoka katika viwanda vya kusindika minofu hiyo kanda ya Ziwa, badala ya kutumia viwanja vya ndege vya nchi za jirani.

Kwa sasa tayari ujenzi wa majengo kwa ajili ya kuhifadhia minofu ya samaki katika uwanja wa ndege wa Mwanza, yanaelekea kwenye hatua ya kukamilika, ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia uwanja huo kibiashara.

Comments

comments