Serikali ya China yaahidi kuhimiza maendeleo yenye ubora zaidi.

Ripoti ya kazi za serikali ya China iliyotolewa leo katika Bunge la Umma imeeleza kuwa, malengo makuu ya mwaka huu ya maendeleo ya uchumi na jamii ya China ni kukuza uchumi kwa asilimia 6 hadi 6.5, kuongeza ajira kwa zaidi ya watu milioni 10, na kudhibiti mfumuko wa bei kuwa karibu asilimia 3. Pia kupunguza watu maskini zaidi ya milioni 10, na kubana matumizi ya nishati kwa kila kiasi fulani cha uzalishaji mali. Ikiwa nchi ya pili kwa ukubwa kiuchumi duniani, hivi sasa China inajitahidi kuhimiza maendeleo yenye ubora zaidi.

Kutokana na ongezeko la mivutano ya kibiashara na vitendo vya kupinga utandawazi duniani, mwaka huu China imepunguza makadirio ya kasi ya ukuaji wa uchumi wake, ili kukabiliana vizuri na changamoto na kudumisha maendeleo mazuri ya uchumi. Hata hivyo, pato la taifa la China la mwaka jana lilifikia dola trilioni 13.6 za kimarekani, na ongezeko la asilimia 6 hadi 6.5 litakuwa kubwa sana, hivyo kuifanya China kuendelea kuwa injini kubwa zaidi ya maendeleo ya uchumi wa dunia.

Ili kutimiza lengo la maendeleo ya uchumi, serikali ya China imepanga kazi kuu kumi kwa mwaka huu, zikiwemo kuendeleza uvumbuzi na kukamilisha njia za usimamizi, kuboresha mazingira ya kibiashara, kuzingatia uvumbuzi katika kuhimiza maendeleo, kujenga soko kubwa na lenye nguvu ya ndani, na kusukuma mbele juhudi za kupunguza umaskini na ustawi vijijini. Kazi nyingin ni kuhimiza uwiano wa maendeleo katika sehemu mbalimbali, kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kukuza mageuzi katika sekta muhimu, kuhimiza ufunguaji mlango kwa pande zote, na kuharakisha maendeleo ya kijamii.

Hivi sasa kutokana na changamoto kubwa za ndani na nje, China inalazimika kufanya juhudi zaidi ili kutimiza malengo ya maendeleo. Wakati ilipopanga kazi za mwaka huu, serikali ya China imesisitiza umuhimu wa kushughulikia vizuri uhusiano kati ya mambo ya ndani na mambo ya kimataifa, uhusiano kati ya kudumisha ongezeko la uchumi na kukinga hali hatari, na uhusiano kati ya serikali na soko.

Huu ni mwaka wa 70 tangu Jamhuri ya Watu wa China ianzishwe. Ingawa mazingira ya kimataifa yanatatanisha, lakini China bado ina fursa nzuri ya kujiendeleza. China itashikilia nia ya kufanya vizuri mambo ya ndani, na kushinda changamoto mbalimbali, ili kuanzisha mustakabali mzuri zaidi.

Comments

comments