Kufuatia shambulizi la mtandao wa internet la kompyuta laki 2. Kijana wa Uingereza azuia kuenea kwa kirusi kibahati

HackerNews

Shambulizi kwenye mtandao wa internet lililotokea ijumaa iliyopita limeathiri zaidi ya kompyuta laki 2 kwenye nchi 150 duniani.

Mkuu wa Shirika la Europol Bw Rob Wainwright amesema wahanga wengi ni wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na mashirika makubwa, na idadi kubwa namna hii ya nchi zilizoshambuliwa haijawahi kutokea.

Bw. Wainwright amesema kuwa shambulizi hilo lilitokea ijumaa, idadi ya wahanga huenda itaongezeka kufuatia watu wanaorudi kazini jumatatu baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki kuripoti.

Russia na Uingereza ndio zimeathiriwa zaidi na shambulizi hilo, na idara za afya ndio zimekuwa mhanga mkubwa. Hata hivyo Bw. Wainwright amesema Europol inachunguza chanzo cha shambulizi hilo kwa msingi kwamba lilifanywa na wahalifu na sio magaidi. Pia amesema si pesa nyingi zilizoibiwa kwenye shambulizi hilo, lakini nchini Uingereza madaktari, manesi na maofisa wengine walishindwa kuangalia mafaili ya wagonjwa.

Mhandisi wa mtandao wa Internet mwenye umri wa miaka 22 kutoka Uingereza asiyetaka kutaja jina lake aligundua kuwa kirusi hiki kimekuwa kikijaribu kutembelea tovuti isiyokuwepo yenye jina la ajabu, hivyo alisajili tovuti hii kwa kutumia pauni 8.5, ili kutafiti data husika za kirusi hiki. Lakini jambo la kushangaza lililotokea, maamubukizi ya kirusi hiki yalisita baada ya tovuti hii kusajiliwa.
Mhandisi huyu amechambua sababu ya kirusi hiki kutembelea tovuti hii. Kama tovuti hii isingekuwepo, inamaanisha kirusi hiki bado kisingetambuliwa na wafanyakazi wa usalama wa Internet, na kingeweza kuenea bila vizuizi vyovyote; lakini kama tovuti hii ipo, inamaanisha wafanyakazi wa usalama wa Internet wametambua uwepo wa kirusi hiki na kuchukua hatua za kukizuia, hivyo inatakiwa kirusi hiki kuacha kuenea ili kuepusha data nyingi zaidi zisipatikane na wafanyakazi hao.
Mhandisi huyu amesema hakujua kama kusajili tovuti hii kungezuia kuenea kwa kirusi hiki, kwani alifanya hivyo kwa bahati tu.
Kampuni ya Maabara ya Kaspersky ya Russia imesema kirusi hiki kimetumia software ya kudukua ya “Eternal Blue” inayotoka kwenye benki ya silaha za mtandao wa Interent ya Idara ya Usalama ya Marekani NSA. Mwezi Aprili mwaka huu, shirika la wadukuzi Shadow Brokers lilidokeza baadhi ya software zinazotumika kudukua za NSA ikiwemo “Eternal Blue”.

Comments

comments