Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimeondoka Alfajiri ya leo kwenda mjini Blomofontein, Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho

Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimeondoka Alfajiri ya leo kwenda mjini Blomofontein, Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.

Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na kuelekea mchezo huo, watakuwa kambini Afrika Kusini kwa siku 10.

Wachezaji waliosafiri na Stars pamoja na makipa Aishi Manula wa Simba , Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.

Mabeki ni Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba, Ally ëSonsoí Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zote za nyumbani.

Viungo ni Salum Abubakar ëSure Boyí, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga , Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba zote za nyumbani na washambuliaji ni Thomas Ulimwengu aliye huru baada ya kuvunja mkataba na Al Hilal ya Sudan mwishoni mwa wiki, John Bocco wa Simba na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili.

Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.

Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.

Comments

comments