Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabili changamoto ya usawa wa kijinsia, ambapo imehakikisha kwa vitendo kwamba wanawake wanapata fursa na usawa unaostahili katika vyombo vikubwa vya maamuzi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Radio Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kwa mara ya kwanza Tanzania imepata Makamu wa Rais Mwanamke, ikiwa ni jitihada ya kuondoa changamoto hii ya usawa wa kijinsia, ambayo bado ni kubwa duniani.

Waziri Ummy Mwalimu anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha 63 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani kilichofunguliwa jijini New York Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Antonio Guterres.

Aidha, Waziri Ummy Mwalimu pia amesisitiza kwamba hata ushiriki na michango ya wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa wa manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi.

Mkutano huo unawaleta pamoja zaidi ya washiriki 9000 kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, yakiwemo mashirika ya UN na yale ya kiraia ambapo wanajadiliana jinsi ya kumkomboa mwanamke, hususan katika nyanja ya uongozi.

Akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Antonio Guterres amebainisha kwamba usawa wa kijinsia bado ni changamoto kubwa duniani, ambapo amesisitiza kwamba dunia inapaswa kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa.

Comments

comments