Biashara ya dawa Miongoni mwa Nchi za SADC.

Changamoto ya wafanyabiashara wa nchi za SADC kulazimika kufanya ukaguzi na kusajili bidhaa wanazotengeneza kwenye kila nchi wanachama wa SADC wanayotaka kwenda kufanya biashara hiyo, imepata ufumbuzi kwa upande wa sekta ya madawa, baada ya miongozo yote ya ukaguzi, usajili na majaribio ya dawa kufanyiwa maboresho na kuwa inayofanana kwa nchi zote wanachama wa SADC.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainabu Chaula ameyasema hayo wakati anafungua mafunzo ya wiki mbili ya wataalamu wa ukaguzi wa viwanda vya dawa kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya SADC, mafunzo yanayoendeshwa na mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kwa ufadhili wa shirika la fedha duniani IMF.

Mafunzo hayo ya nadharia na vitendo, sasa yanawezesha zoezi zima la nchi wanachama wa SADC kuwa na lugha moja katika masuala ya ukaguzi wa viwanda vya dawa na hivyo kuondoa urasimu kwenye umoja huo katika suala la biashara kwenye sekta ya dawa.

Je baada ya kukamilika kwa utaratibu mzima wa utendajikazi wa ukaguzi wa viwanda vya dawa kwa nchi wanachama wa SADC, wafanyabiashara kwenye sekta ya dawa ndani ya SADC watarajie nini?

Pamoja na kwamba mkutano wa 39 wa SADC unafanyika hapa nchini, Tanzania kupitia TMDA imeandaa mafunzo hayo ya wiki mbili kwa watalaamu wa ukaguzi wa viwanda vya dawa chini ya ufadhili wa shirika la fedha duniani, kwa nchi zote wanachama wa SADC kufuatia Tanzania kuwa nchi pekee barani afrika ambayo ina ngazi ya tatu katika umahiri, wa kuwa na mifumo ya udhibiti wa dawa hivyo ina watalaamu waliobobea kwenye sekta hiyo.

Comments

comments