Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atoa tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi pia kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.

Amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Waziri Mkuu ameyasema hayo katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.

Amsema Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja.

Pia, Waziri Mkuu amsema Serikali imeendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za Sekondari, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Polisi, Hospitali za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program yao ya Seed of the Futureambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa.

Amesema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.

Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini.

Comments

comments