Usajili wa Kadi za simu, TCRA yatoza faini 10.74 Bilioni kwa makampuni ya simu za mkononi

SIMU ZA MKONONI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imeyatoza faini jumla ya shilingi bilioni 10.74 makampuni ya simu za mkononi kwa kosa la kukiuka sheria, kanuni na taratibu na kanuni za usajili wa kadi za simu hususan katika nyakati hizi ambapo uhalifu unaenda kidigitali.

TCRA wamesema faini hizo zinatakiwa kulipwa ifikapo au kabla ya Oktoba 14 mwaka huu.

Katika faini hizo kiwango cha juu kilichotozwa kwa kampuni moja ni shilingi bilioni 2.9 na kiwango cha chini ni milioni 600.

Kadi hizo za simu ni zile ambazo aidha zilisajiliwa namba za simu bila vitambulisho vya wateja, kusajili namba bila ya kuwa na picha za wateja wenye namba hizo, ama kutokuwa na sahihi ya wateja na kutumia kitambulisho cha mtu mwingine jambo ambalo limetajwa kuwa linahatarisha usalama wa taifa na raia kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wawakilishi wa makampuni ya simu Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba amesema kiasi hicho cha fedha kimejumuisha faini ambayo imetozwa kwa kuzingatia kwamba si mara ya kwanza kwa makampuni hayo kukiuka sheria, na ndani yake kiasi cha shilingi milioni 500 kwa kila kampuni italipwa kwa TCRA kwa kuathiri na kuhatarisha usalama wa umma na jamii ya watanzania.

Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo wa TCRA ametoa wito kwa yeyote atakayehitaji kununua kadi ya simu ahikishe anasajili kikamilifu ili kuepuka mkono wa sheria.

Comments

comments