UZINDUZI RASMI PROGRAM YA MAFUNZO LUGHA YA KIINDONESIA

Program ya mafunzo ya lugha ya Kiindonesia ambayo itafundishwa katika chuo cha Diplomasia imezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam.

Akizindua program hiyo balozi wa Indonesia hapa nchini Prof. Ratlan Pardede ameelezea kufurahishwa na mwitikio wa Watanzania wengi ambao wameonyesha ari ya kutaka kufahamu lugha hiyo kama njia ya mawasiliano ambayo itaendeleza kudumisha ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia

Balozi huyo wa Indonesia amewataka wanafunzi kuwa na utayari wakati wa mafunzo wa lugha hiyo ambayo itakuwa na manufaa kwao kwani fursa ya kufahamu lugha nyingi za kigeni pia inasaidia taifa hususani katika soko la ajira. Aidha amekipongeza Chuo cha Diplomasia kwa kufanya jitihada kuanza kufundisha lugha hiyo.

Awali akimkaribisha balozi huyo kuzindua mafunzo hayo ya Lugha ya Kiindonesia Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia Dkt.Jeremia Ponera aliishukuru Serikali ya Indonesia kupitia ubalozi wake hapa nchini kwa kuona umhimu wa kukitumia Chuo cha Diplomasia kama kituo cha mafunzo ya Lugha ya Kiindonesia na kwamba kuanza kwa mafunzo hayo kunatokana na mashirikiano mazuri ya Tanzania na Indonesia ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, pamoja na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Indonesia Mhe. Joko Widodo wameendelea kuyadumisha

Amesema kuwa mpango wa muda mrefu wa Chuo hicho ni kuona kinafikia dira yake ya kuwa kituo bora kikanda katika mafunzo ,utafiti, machapisho, na utoaji wa ushauri wa kitaalamu katika nyanja za mahusiano ya Kimataifa ,kidiplomasia na utatuzi wa migogoro pamoja na ujenzi wa amani

Comments

comments