Watanzania wameaswa kujiwekea utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara na kuepuka matumizi ya dawa za kutuliza maumivu kiholela zinazotajwa kuwa miongoni mwa visababishi vya ugonjwa wa figo.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na watoto, Dkt. Faustine Ndungulile wakati akizungumza na wanahabari kuhusu siku ya figo duniani inayoadhimishwa kila Machi 14.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu waziri Dkt. Ndungulile amesema kuwa miongoni mwa visababishi vya ugonjwa wa figo nchini ni pamoja na kutofanya mazoezi, huku kasi ya ongezeko la matumizi ya dawa za kutuliza maumivu kiholela ikiwa pia sababu ya ugonjwa huo.

Aidha Naibu waziri amesema gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja wa magonjwa ya kuambukiza ni nafuu kulinganisha na yale yasio yakuambukiza ikiwamo kisukari, ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu pamoja na Figo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo, ambaye pia ni rais wa chama cha madaktari wa figo nchini Dkt. Onesmo Kisanga anaeleza kuwa bado ugonjwa huu ni tishio kwa nchi za kusini mwa jangwa la sahara, huku utafiti uliofanyika ngazi ya kaya kaskazini mashariki mwa Tanzania ukionyesha kuwa asilimia 6.8 wana matatizo sugu ya figo.

Comments

comments