Waziri Prof. Kabudi amekabidhiwa uenyekiti wa Baraza la Mawaziri SADC.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amekabidhiwa uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, ikiwa ni hatua za Tanzania kuelekea kuwa mwenyekiti kamili wa jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja ujao.

Hiyo ni ishara ya makabidhiano, ambapo Prof Kabudi amepokea kijiti kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi Naitwah aliyemaliza muda wake ikiwa ni sehemu ya mkutano wa mawaziri utakaohitimishwa na wakuu wa nchi wanachama Agosti 17 na 18 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Prof. Kabudi amesema kwa mujibu wa kaulimbiu ya mkutano huu iliyotolewa na Tanzania, isemayo Maendeleo Shirikishi kwa ajili ya Maendeleo ya viwanda endelevu katika kuongeza biashara ya kikanda na kuongeza ajira, kaulimbiu ambayo itaongoza uenyekiti wa SADC ndani ya mwaka mmoja ujao, na kwamba Tanzania itasimamia kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu, kuongezeka biashara kikanda pamoja na ajira.

Prof Kabudi amesisitiza kuwa Tanzania katika uenyekiti wake pia itaendeleza harakati za kuitaka jumuiya za kimataifa kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.

Mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake Netumbo Nandi Ndaitwah amehimiza baraza hilo kuendelea kujipanga katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha majanga ya asili, kama ilivyotokea wakati wa vimbunga Idai na Kenneth vilivyosababisha madhara makubwa katika nchi nyingi za jumuiya hiyo.

Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax amezungumzia umuhimu wa kuweka msukumo katika biashara ndani ya jumuiya hiyo ambapo kwa sasa biashara baina ya nchi wanachama wa SADC ni chini ya asilimia 20.

Baadhi ya kazi za baraza la mawaziri la SADC ni pamoja na kuangalia maendeleo ya utendaji, utekelezaji wa sera na miradi ya jumuiya na kushauri wakuu wa nchi na serikali katika masuala ya kisera ikiwemo kuweka usawa katika utekelezaji wa makubaliano sera na mikakati ya jumuiya hiyo.

Comments

comments