Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wana matumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda leo uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewaeleza wachezaji hao kuwa Serikali ina imani nao na kwamba wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani, hivyo akawataka wakapigane kufa na kupona ili kupata ushindi na hatimaye kufuzu.

Taifa Stars kupitia Nahodha wake Mbwana Samata wamemwahidi Waziri Mkuu kwamba watapigana kufa na kupona kuhakikisha kwamba wanatibu kiu ya Watanzania kwa kupata ushindi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa shilingi milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), na kuongeza kwamba watanzania wanaamini kwamba safari hii ni zamu yao kushiriki fainali hizo.

Nae, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala ameahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda hivyo akawataka wachezaji hao wakapiganie Taifa lao.

Comments

comments