Waziri Angela Kairuki amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji kwa Wawekezaji na Wafanyabishara wa ndani na nje ya nchi.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angela Kairuki amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji kwa Wawekezaji na Wafanyabishara wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuhakikisha vikwazo vilivyokuwa vinawakabili ikiwemo urasimu katika utoaji vibali na upatikanaji wa ardhi vinatokomezwa.

Waziri Kariuki pia ametoa rai kwa Watanzania wenye maeneo makubwa ya ardhi kuyatoa maeneo hayo kwa ajili ya wawekezaji wenye uhitaji wa kukodi ama kununua ili kuyaendeleza kwa shughuli za uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari alipokutana an ujumbe wa Kundi la Wafanyabishara kutoka Hongkong China walioko nchini kwa ajili ya kutafiti maeneo ya Uwekezaji Waziri Kairuki amesema kuwa kwa sasa Tanzania imekuwa ikipokea makundi mbalimbali ya wawekezaji kutoka nje wenye nia ya kuwekeza nchini katika sekta na maeneo mbalimbali hivyo Serikali iko katika kasi ya kuboresha na kuweka mazingira rafiki yatakayovutia zaidi wawekezaji hao huku akizitaka Taasisi nyingine za serikali kuhakikisha zinahudumia wawekezaji hao kwa kasi na weledi

Aidha akizungumzia ujumbe huo wa Hongkong Waziri Kairuki amesema kuwa wafanyabishara hao wanatafuta maeneo ya Uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha dawa za binadamu pamoja na vifaa tiba, ununuzi wa Ufuta na majani yake kwa ajili ya kuuza nje ya nchi pamoja na Uchakataji korosho ambapo tayari wameshatembezwa maeneo kadhaa na kuridhishwa na mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) amesema kituo hicho kitazidi kuimarisha mahusinao ya Kibiashara na HongKong ambapo mpaka sasa wamekwishafanya mazungumzo na Mamlaka ya Biashara na Uwekezaji ya Hongkok kuhusiana na makubaliano ya kuhakikisha wafanyabishara na wawekezaji toka Hongkong wanatumia fursa za uwekezaji za nchini Tanzania pamoja na wenzao kutokana hapa nchini kwenda Hongkong kufanya uwekezaji.

Comments

comments