Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 ambapo asilimia 81.50 ya watahiniwa 933,369 wamefaulu mtihani huo huku watahiniwa 909 wakifutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu.
Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt. Charles Msonde amesema kwa jumla matokeo hayo yanaonyesha ufaulu umeongezeka kwa asililia 3.78 lakini ufaulu katika somo la Kiingereza bado ni mdogo ikilinganishwa na masomo mengine.
Aidha Dkt Msonde ameziomba mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua kali za kisheria wasimamizi wa mitihani na walimu waliohusika kuvujisha mitihani kwa kuwa wanarudisha nyuma juhudi za kuboresha sekta ya elimu nchini
Katika matokeo hayo, Grace Imori Manga wa shule ya msingi Graiyaki ya mkoani Mara ametangazwa kuwa wa kwanza kitaifa akifuatiwa na Francis Gwani wa shule ya msingi Paradise ya mkoani Geita na namba tatu imeshikiliwa na Loi Kitundu wa Shule ya msingi Mbezi ya Dar es Salaam.