Wakati huu ambapo ligi za soka nchini zinatarajia kurejea baada ya Taifa kujiridhisha na mafanikio yaliyopatikana dhidi ya janga la Corona, tayari wachezaji pamoja na timu zao wameanza hatua muhimu za kujianda ikiwemo kuingia kambini pamoja na mazoezi.
Mapema leo jijini Dar es Salaam wachezaji wa klabu ya Simba wameonekana wakiitikia wito wa kufika katika kambi ya timu hiyo iliyopo maeneo ya Mbweni jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine wanatarajiwa kuanza mazoezi baada ya taratibu zote za kurejea kukamilishwa.
Inaelezwa kuwa wachezaji hao watapitia hatua zote za msingi zilizowekwa kulingana na maagizo ya serikali chini ya usimamizi wa idara za afya, ikiwemo kuchukuliwa vipimo vya afya ikiwa ni hatua tahadhari, lakini pia benchi la ufundi likitarajiwa kuwapokea kwa kufuata makubaliano yake na wachezaji hao.
Timu hiyo ambayo ndiyo mabingwa watetezi na vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara inatarajia kuanza mazoezi katika uwanja wake wa MO-ARENA Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salam.