Marekani imeiamuru China kufunga ubalozi wake mdogo mjini Houston, Texas ifikapo ijumaa wiki hii, hatua ambayo imetafsiriwa na China kuwa uchokozi wa kisiasa.
Idara ya utawala ya Marekani imesema uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda haki bunifu ya taaluma ya Marekani.
Lakini waziri wa mambo ya nje wa China Wang Wenbin amesema kitendo hicho kinaudhi na hakikubaliki.
Uamuzi huu umefikiwa baada ya watu wasiofahamika kupigwa picha wakichoma nyaraka mbalimbali kwenye vyombo vya kuhifadhia uchafu katika eneo la jengo la ubalozi huo.
Mvutano kati ya Marekani na China umekuwa ukiongezeka kwa muda sasa, ambapo utawala wa Rais Donald Trump umekuwa ukigongana na taifa hilo katika eneo la biashara, chanzo cha ugonjwa wa Covid-19 pamoja na hatua ya China kuweka sheria mpya ya usalama Hong Kong.