Rais Dkt. Magufuli aongoza kuaga Kitaifa mwili wa Hayati Mzee Mkapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Taifa limepoteza hazina kubwa kufuatia kuondokewa na Hayati rais mstaafu wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuwa alikuwa kiongozi Mahiri, shupavu mchapakazi ,Mzalendo, asiyeyumbishwa ambaye alisimamia ukweli na uwazi.

Mhe. Rais Magufuli amesema serikali anayoiongoza itaendelea kuyaenzi yote mema yaliyoanzishwa na kiongozi huyo kwa maendeleo na ustawi wa taifa.

Ni mwili wa Rais Mstaafu hayati Benjamin William Mkapa ulipowasili katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam majira ya asubuhi kwa ajili ya kuagwa rasmi kitaifa baada ya ibada ya Misa Takatifu ya kumwombea iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Immaculate lililopo Upanga.

Mara baada ya kuwasili, wimbo wa Taifa ukapigwa kyashiria kuanza kwa kuaga kitaifa mwili wa hayati Mzee Mkapa, ambapo akihutubia waobolezaji Mhe Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa pamoja na mambo mengi aliyoyafanya Hayati Rais Mstaafu Mkapa akiwa kiongozi wa Taifa pia alikuwa ni baba wa demokrasia kwani alikuwa Rais wa kwanza kuingia Madarakani kupitia Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliohusisha vyama vingi tangu kurejeshwa kwa mfumo huo.

Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya kuingia Madarakani Mzee Mkapa alifanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ikiwemo ya kuendeleza sekta binafsi pamoja na kufanya jitihada kubwa ya kupambana na madeni ya nje, ambayo yalifanikisha Tanzania kufutiwa sehemu ya madeni hayo kupitia mpango wa HIPC lakini aliamini kuwa ili nchi iweze kusonga mbele ni lazima kujitegemea.

Wakitoa salaam za rambirambi, baadhi ya wawakilishi wa nchi za nje akiwemo Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume wamesema Kifo cha Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ni pigo kubwa si kwa Tanzania pekee, bali kwa jumuiya nzima ya kimataifa kwa kuwa alikuwa ni mwanadiplomasia mahiri aliyetumia muda wake kutatua migogoro katika nchi mbalimbali na kuchochea maendeleo kwa misingi ya haki.

Awali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa aliwataka wananchi kuendelea kumuombea kiongozi huyo huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi akielezea wasifu wa Hayati Benjamin William Mkapa uliosheheni utumishi wake kwa taifa, kikanda na jumuiya ya kimataifa.

Hayati Benjamin Wiliam Mkapa alizaliwa tarehe 12 Mwezi Novemba mwaka 1938 na kabla ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu alishika nyadhifa mbalimbali utumishi naza uongozi ikiwemo Mhariri wa magazeti ya serikali na chama, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria,Canada na Marekani,Waziri wa Mambo ya nje pamoja na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu ambapo alifariki dunia Julai 23 mwaka huu jijini Dar es salaam.

Comments

comments

Clement Silla

Read Previous

Wasimamishwa kupisha Uchunguzi wa TAKUKURU.

Read Next

Mzee Mkapa azikwa Kijijini kwake Lupaso Mtwara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!