Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imemfungia miaka miwili na faini ya Shilingi milioni 3 aliyekuwa kocha wa klabu ya Yanga Luc Eymael kwa kosa la kutoa maneno ya Kibaguzi wakati Yanga ilipocheza na Lipuli katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika makao makuu ya TFF maeneo ya Karume Jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya shirikisho hilo Wakili Alex Mshumbushi amesema adhabu hiyo imetolewa kwa kufuata kanuni za uendeshaji wa ligi kuu kipengele cha udhibiti wa makocha.
Mbali na adhabu hiyo iliyotokana na kosa la Ubaguzi, Kamati ya nidhamu pia imempiga faini nyingine kiasi cha shilingi milioni tano kocha huyo raia wa Ubelgiji kwa kosa la kuishutumu TFF kuwa inaipendelea klabu ya Simba ambapo ushahidi wa kosa hilo ulifikishwa kwenye kikao cha kamati cha Agosti Mosi mwaka huu na kujiridhisha.
Kwa niaba ya kamati ya Nidhamu ya TFF, Wakili Mshumbushi ametoa onyo kwa makocha, na kuwataka kuacha mara moja vitendo vyote vyenye vinasaba vya kibaguzi ambayo yanachagua taswira ya soka la Tanzania.