Waziri Mkuu Tanzania azindua uchepushaji wa maji ya Mto Rufiji.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua uchepushaji wa maji ya Mto Rufiji kwenda kwenye handaki ili kuruhusu ujenzi wa tuta kuu kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere uliopo Rufiji mkoani Pwani.

Ni mradi mkubwa wa kimkakati unaoiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye mabwawa makubwa duniani yanayozalisha umeme wa maji, huku ukiakisi ndoto za baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kupitia maono ya Rais wa awamu ya tano mh Dkt. John Pombe Magufuli, Tanzania kuwa na umeme mwingi wa kutosha.

Akizungumza katika hafla fupi iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali, baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji, mh Majaliwa amesema kukamilika kwa mradi huo, kutachochea mapinduzi ya sekta ya viwanda nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

Mh Majaliwa amesema mradi huo ni kielelezo cha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na serikali ya Misri, hasa kutokana na kwamba unatekelezwa na makampuni mawili kutoka Misri Arab Contractors na El Sewedy Electric.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu, mradi huo ulikuwa umeshatoa ajira za moja kwa moja 6,364 ambapo kati ya hizo, ajira 5,728 zikiwa ni za Watanzania.

Awali aliyekuwa waziri wa Nishati, Dkt. Merdad Kalemani alisema mradi huo unaoatarajiwa kukamilika Juni 2022 ni wa kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki lakini ni wa nne kwa ukubwa barani Afrika na hadi sasa Sh trilioni 1.7 zimeshalipwa kulingana na kiwango cha kazi, huku Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka akisema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 75.76.

Kwa upande wake Waziri wa Umeme na Nishati wa Misri, Dkt. Mohamed Shaker El-Markabi amesema Serikali ya nchi hiyo iko tayari kubadilishana uzoefu na wizara ya nishati ya Tanzania na kwamba itatoa mafunzo kwa Watanzania 25 kwa miaka mitatu ijayo.

Comments

comments

Clement Silla

Read Previous

Serikali ya Ethiopia yadai kuukamata Mji wa Alamata.

Read Next

Rais Mwinyi afanya ziara yakushtukiza hospitali ya Rufaa ya Mnazi moja Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow On Instagram
error: Content is protected !!